Friday, October 20, 2017

BLOG YA MAISHA YA MAFANIKIO IMEONA HII PICHA IWE PICHA YA WIKI..KWA VILE...

Imenkumbusha Kapulya mimi  mengi sana wakati nikiwa shule ya msingi...hakuna kuongea kilugha shuleni. Kulikuwa na tabia wanafunzi kuongea sana kilugha mashuleni enzi zangu. Basi walimu wakabuni ya kwamba watengeneza aina ya kakibao kadogo kalikoandikwa hakuna kuongea  kilugha kwa mfano kingoni...basi ukijisahau unaongea unavalishwa kile kibao na mwisho wa siku mwalimu wa zamu anatangaza wote waliovaa/valishwa kile kibao wajitokeze na hapo wote ni bakola tu...Lakini unafikiri kesho yake wale waliochapwa waliacha kuongea kilugha aaahh wapi....Hiki kibao nimekumbuka  jinsi wanafunzi walivyokuwa wanapata mateso... Je nawe una kumbukumbu yoyote ile inayofanana na hii?...KAPULYA wenu....

Thursday, October 19, 2017

KUMBUKUMBU:- STADI/MFUMO WA MAISHA YA JAMII ZETU

Mabinti wakitoka kutafuta kuni mwituni...nimekumbuka mbali sana, siku hizi sijui kama kizazi cha sasa wanajua kuni ni nini?
na hapa ni usafiri wetu.

Wednesday, October 18, 2017

MSIMU WA JOTO WAELEKEA KIKOMO NA PIA KILIMO KWA HIYO IMENIBIDI NIZICHUME NYANYA ZANGU NA KUZIHIFADHI NDANI....

HAPA HIZI ZAONYESHA MAFANIKIO KIDOGO
 Na hapa sijui zitaiva au zitaoza? mwenye MBINU nyingine TAFADHALI nisaidieni...natumaini nitapata msaada toka kwenu...natanguliza shukrani

Kwa pilipili sina mashaka 

Sunday, October 15, 2017

DOMINIKA YA ISHIRINI NA NANE YA MWAKA A

NIMETUMIWA HII NA RAFIKI NIMEONA NI VEMA NIIWEKA HAPA KIBARAZANI ILI WENGI TUPATE KUJUA ...

MASOMO.
Isa.25 :6-10.
Flp.4:12-14,19-20.
Injili Mt 22: 1-14.

WAZO KUU: HAITOSHI TU KUBATIZWA NI LAZIMA PIA KUUISHI  UBATIZO.
UTANGULIZI.
Ndugu zangu leo ni Dominika ya Ishirini na nane ya mwaka A wa kanisa.Tumefika tena siku ya Bwana ili kumsikiliza na kumwabudu.Leo Masomo yetu yanatufakarisha juu ya mwaliko wa Mungu kwa wanadamu wote.Bwana Mungu anawaliaka watu wote kushiriki furaha ya heri ya milele.Mwaliko huo ni wa bure,kuuitikia ni heri,na kuukataa ni hasara kubwa kwa kukosa vinono kwenye karamu ya Mbinguni.Tumuombe Mungu atujalie neema zake ili kukubali mwaliko wake na kubaki katika kanuni za mwaliko huo daima.Tutafakari masomo yetu tukiongozwa na wazo hili,Haitoshi tu kubatizwa ni Lazima pia kuuishi Ubatizo.

UFAFANUZI.
Ndugu zangu,katika somo la kwanza nabii Isaya anaeleza uzuri wa karamu ya Bwana aliyowaanadalia watu wake.Bwana Mungu anawaalika watu wote kwenye sherehe yenye vitu vingi vizuri.Kwanza Mwaliko ni kwa watu wa Mataifa yote.Kutakuwa na vyakula vingi vinono, vilivyandaliwa juu ya mlima wake Mtakatifu.Pili kutakuwa na  uchangamfu mwingi, maana utaji uliotandwa nyusoni mwa watu kwasababu ya huzuni utaondolewa.Tatu Kutakuwa na furaha tele maana hakutakuwa na mauti tena kwa sababu Bwana ataangamiza mauti, kuyafuta machozi ya watu wake,na kuwaondolea aibu yao.

Katika Injili tumesikia Yesu akitoa mfanano wa Ufalme wa Mbinguni kwa Mfano wa Sherehe ya Harusi.Anasema Ufalme wa Mbinguni umefanana na mwaliko wa mfalme aliyewaalika watu kwenye karamu ya harusi ya mwanae.Walioalikwa  walikataa.Akatuma tena watumishi wake kuwaita walioalikwa wafike,vinono ni tayari.Hawa  hawakujali,wakatoa udhuru kuwa wamebanwa na shughuli zao wakaenda kwenye shughuli zao na waliosalia wakawakamata na kuwaua watumishi wa mfalme.Mfalme alikasirika na kuwaangamiza waalikwa wale walitenda mabaya hayo pamoja na mji wao.Kisha aliwatuma watumishi wake kuwaita hata waliokuwa wapitaji tu wa Barabarani ili harusi ijae watu.Harusi ikajaa wageni.Hivyo waalikwa wa kwanza si tu walikataa mwaliko bali pia waliwaua wajumbe waliotumwa kutoa ujumbe wa mwaliko.Nafasi yao ikachukuliwa na waalikwa wa awamu ya pili.Hawa nao waliofika  mmoja hakuwa na vazi la harusi.Alipohojiwa na Mfalme kuwa ameingiaje kwenye harusi bila vazi la harusi? Huyu hakuwa na la kujitetea.Basi Mfalme akaamuru huyu afungwe mikono na miguu na kutupwa nje.

Katika somo la pili mtume Paulo anasema anafaulu kufanya mambo mepesi na magumu kwa sababu ya nguvu ya Kristo anayopata toka kwa Kristo mwenyewe.Anasema anayaweza yote katika Kristo amtiaye nguvu.Anawashukuru wafilipi kwa ukarimu wao kwake kwa msaada waliompatia na anawaombea baraka ya Mungu.

MAISHANI.
Ndugu zangu,mwaliko wa Mungu ni mwaliko wa neema.Tumealikwa kushiriki heri na furaha ya milele bila mastahili yetu.Kama wale walioalikwa toka mwanzo au wale  walialikwa toka  barabarani hawakutarajia kupata mwaliko ule wala hawakufanya chochote ili waalikwe,vivyo hivyo tunaalikwa kushiriki heri ya Mbinguni kwa sababu ya upendo wa Mungu kwetu.Masomo haya yanatutafakarisha maisha yetu ya kikristo.Baada ya kukubali mwaliko wa imani  na kuupokea ubatizo tujue kwamba tunapaswa kuuishi Ukristo wenyewe.Masomo yanatukumbusha kwamba:

Mungu anawaalika watu wote kwenye heri ya Milele Mbinguni.Pamoja na kuwa mwaliko huo wa Mungu ni mwaliko wa furaha kati ya waalikwa hao,wapo wanaokubali na wapo wanaokataa kama ilivyo kwenye mfano wa Harusi.Ni bahati,heri na furaha kualikwa na Mungu.Wale wanaokataa mwaliko wa Mungu wanapata hasara kubwa sana.Ubaya mkubwa wa kuukataa mwaliko wa Mungu si adhabu au mateso atakayopata aliyekataa mwaliko bali ni Kukosa uzuri na vinono vya sherehe ile.Mimi nafikiri ni mateso makubwa sana kukosa kupata kilicho kizuri kuliko vyote na bila tumaini la kukipata tena.Hilo ni teso baya.Pamoja na kuadhibiwa kwa kupata mateso ni kibaya zaidi kukosa vinono.

Tukumbuke kwamba vyenye uzuri visichukue nafasi ya uzuri Mwenyewe.Maana vitu vizuri vimetoka kwa uzuru mwenyewe yaani Mungu.Tusifikiri kwamba mambo yanayoweza kusababisha tusiitikie mwaliko wa Mungu si lazima yawe mabaya.Tumesikia kuwa waalikwa wengine wa kwenye harusi hawakujali mwaliko wa Mfalme,wengine wakaenda shambani na wengine kwenye biashara zao.Si jambo baya kwenda shambani kufanya kazi wala kwenda kwenye biashara,maana hizo ni kazi za mtu kujipatia mkate wake wa kila siku.Ni mambo yaliyo mazuri.Lakini tusisahau kwamba haifai kujishughulisha na mambo mazuri na kumuacha Mungu aliye uzuri wenyewe.Mambo mazuri yanashirikishwa tu sehemu ya uzuri wa Mungu.Mungu ndiyo uzuri wenyewe.Haifai kujishughulisha na kazi za Bwana tukimuacha Bwana wa kazi.

Haitoshi tu kubatizwa ni lazima kuuishi Ubatizo.Tumesikia kuwa wale waliokubali mwaliko wa Harusi na kuingia harusini ,mmoja hakuwa na vazi la harusi.Kilichompata ni kutupwa nje ya ukumbi akiwa amefungwa mikono na miguu.Tulipobatizwa tuliitikia mwaliko wa Mungu.Ni lazima kuendelea kuvaa vazi la ukristo kwa kuuishi Ukristo wenyewe.Vazi la Harusi,yaani vazi la Ukristo wetu ni matendo mema,maisha ya fadhila.Haifai kabisa kuingia katika ukristo na  kuendelea kuvaa mavazi tuliyokuwa nayo kabla ya kubatizwa yaani kuendelea na maisha ya matendo mabaya,maisha ya vilema.Mfalme aliyetualika anataka kutuona na mavazi ya harusi.Tukiingia na mavazi yasiyo,basi tutatupwa nje hata kama tulikubali mwaliko.Tutatupwa nje hata kama ni wakristo.Haitoshi tu kubatizwa ni lazima kuuishi Ukristo.

HITIMISHO.
Hatimaye ndugu,tumalizie tafakari yetu tukijifunza ukarimu kwa watu wote hasa masikini na fukara.Injili inaeleza juu ya mwaliko wa Mfalme kwa watu ili washiriki harusi.Aliandaa vinono vingi kwaajili ya wageni wake.Tunajifunza ukarimu mkubwa wa Mfalme.Jambo hili litukumbushe kuwa mafiga matatu ya kutusaidia kuuishi vizuri ukristo wetu ni kujisomea na kutafakari  Neno la Mungu,Kupokea Sakramenti za kanisa  hasa Ekaristi na kitubio mara nyingi ,na kutenda matendo ya huruma ya mwili na ya roho.Mimi nafikiri haya mafiga matatu ni msaada mkubwa wa kujivalia vazi la harusi ili tusije tupwa nje maana haitoshi tu kukubali mwaliko wa harusi,ni lazima pia kuvaa mavazi ya harusi.

Tumsifu Yesu Kristo!
Na Padre Augustino Kamnyuka.
Parokia ya Kristo Mfalme Bologna-Italia.
Tarehe 15.10.2017.

Thursday, October 12, 2017

YA KALE NI DHAHABU...YAANI YA KITAMADUNI HASA

Ebu tuangalie kuanzia mavazi hadi mitindo ya nywele ...nimependa sana hii. Yabidi tuienzi ndugu zanguni...
...hapa pia ule mtindo wa kutwanga watatu watatu nimekumbuka mbali sana ...yaani mpaka raha..

Tuesday, October 10, 2017

HAYA MATUNDA NI MATAMU SANA....YANAITWA MAPERA

 Mapera yakiwa mtini na hapo unaweza kujua lipi lipo tayari kuliwa.... kuna wengi wanashindwa kula mapera kutokana na kuwa na .....
....mbegumbegu kama uonavyo hapa...basi ni bora kunywa juisi  yake ni tamu sana....Nimeyatamani sana mapera leo....Je kuna tunda wewe umelitamani kwa hivi karibuni?

Wednesday, October 4, 2017

TAFAKARI YA LEO...MWANAMKE ASIYE NA UPENDO KWA NDUGU WA MUME WAKE

Mwanamke asiyekuwa na upendo kwa ndugu wa mume wake tazama mumewe alichomfanyia................  

Siku moja wakiwa wamekaa pamoja mume pamoja na mke wake mume akamwambia mke wake

 "Mke wangu nimewakumbuka sana ndugu zangu (kaka zangu dada zangu na hata baba na mama) tujumuike pamoja na kula pamoaj,,,,

Kesho nitawaalika ili tujumuike nao katika chakula cha mchana, itabidi uandae chakula kwa ajili yao."

Mke akasema kwa unyonge "Sawa mungu akipenda."

Asubuhi ya siku iliyofuata mume akatoka kwenda katika mishughuliko yake lakini baada ya masaa kadhaa akarejea nyumbani na kumuuliza mke wake.

"Mke wangu umeandaa chakula cha mchana kwa ajili ya wageni? maana baada ya kama muda wa saa moja watakuwa wameshafika."

Mke akajibu "hapana sijapika kwani ndugu zako sio wageni hapa watakula chochote watakachokikuta."

Mumewe akamwambia "Mwenyezi Mungu akusamehe mke wangu kwa nini unayasema hayo ilihali tokea jana nilikuambia ya kuwa wazazi wangu wanakuja

Na kwa nini hukuniambia mapema kuwa hutopika ilihali baada ya muda wa  saa moja wazazi wangu watakuwa hapa nini unafanya mke wangu."

Mke akamjibu "waache waje nitawataka radhi kwani wao si wageni hapa watakula chochote watakachokikuta."

Basi mume ikambidi aondoke pale nyumbani kwa kukwepa fedheha.

Baada ya dakika kadhaa mlango ukagongwa mke akaenda kuufungua.

Kwa mshangao mkubwa alipofungua mlango akakuta wageni waliokuja hapo ni wazazi wake babaake mamaake dada zake pamoja na kaka zake.

Akashtuka kwa mshangao na kuwakaribisha ndani,

Baba akamuuliza kuwa mume wake yupo wapi?

Akajibu yule mwanamke, kuwa alikuwepo hapa ametoka dakika chache kabla hamjafika.

Baba akamwambia "mumeo jana alitupa taarifa kuwa, leo anatuarika hapa tuje kula pamoja chakula cha mchana sasa vipi yeye ametoka si busara."

Yule mwanamke akashtuka kwa taarifa hiyo na kuanza kujifikicha mikono yake huku akiipiga piga hali ya kuchanganyikiwa."

Ikambidi aingie ndani na kumpigia simu mume wake akamwambia "kwa nini hukuniambia kuwa wazazi wangu ndio wanaokuja?"

Mumewe akamjibu "Wazazi wangu na wazazi wako wote ni kitu kimoja/hawana tofauti."

Mke akamwambia "Lete chakula huku chakula kilichokuwepo ni kichache hakitawatosheleza."

Mume akamjibu "Mimi nipo mbali na hao si wageni watakula chochote kilichopo kama wewe ulivyokuwa ukitaka kuwalisha wazazi wangu.

Hili liwe ni somo kwako juu ya kuwaheshimu wazazi wangu."

*Watendee watu kama vile unavyopenda kutendewa wewe* _Tafakari  na chukua hatua_

Tuesday, October 3, 2017

KILIMO CHA KARANGA...KULE KWETU LITUMBANDYOSI KINALIMWA SANA

Karanga ni moja ya jamii ya kunde kwa wale wasiojua ila sidhani kuna mtu hajui karanga ni nini. Karanga hulimwa kwa lengo la chakula, kutengeneza mafuta  pia kwa ajili ya malisho ya mifugo.

Monday, October 2, 2017

NIMEKUMBUKA MBALI SANA....MAPISHI YA UGALI KWA MTINDO HUU

KUMBUKUMBU:- Mafiga matatu  ni mtindo uliozoeleka sana kwa jambo la mapishi  hasa sisi tuliokulia vijijini...HAYA KILA LA KHERI. JUMATATU NJEMA.

Friday, September 29, 2017

TEMBO ZAIDI YA LA KI MOJA WAMEUAWA KATIKA HIFADHI YA SELOUS MKOANI RUVUMA


Hayo yamebainishwa katika maadhimisho ya siku ya tembo kitaifa katika mji mdogo wa LUSEWA wilayani NAMTUMBO mkoani ruvuma katika pori la hifadhi ya wanyama pori SELOUS

Thursday, September 28, 2017

HII IWE PICHA YA WIKI....KATIKA WANYAMA NIWAPENDAO TWIGA NI NAMBA MOJA....

Wiki inakaribia kwisha sasa leo ni ALHAMIS nami nimeona hii iwe picha ya wiki hii sio mbaya kama ikiwezekana kufanya utalii wa ndani ili kupumzisha akili...
Chanzo cha picha ni kutoka kwa blog ya Mjegwa.  PANAPO MAJALIWA TUTAONANA. UJUMBE: TUKUMBUKANE SISI  SOTE NI WANANDUGU

Monday, September 25, 2017

WIKI HII TUANZE NA ZILIPENDWA KWA NJIA YA UJUMBE WA MZIKI


NAWATAKIENI WOTE MWANZO MWEMA WA SIKU AMBAYO KILA WIKI INAANZA NA JUMATATU:-) KAPULYA WENU.

Friday, September 22, 2017

BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO IMECHAGUA HII PICHA IWE PICHA YA WIKI

Napenda kuwatakieni wote mtakaopita hapa mwanzo mwema wa mwisho wa wiki tusisahau kutakiana hali, kwani salamu ni nusu ya kuonana...PANAPO MAJALIWA TUTAONANA TENA AMANI NA FURAHA ITAWALE MIOYONI  MWENU. MNAPENDWA WOTE!

Thursday, September 21, 2017

MAZINGIRA NA BARABARA ZAKE MKOANI RUVUMA....TUTAFIKA KWELI?


Barabara ya Lituhi-Songea yafungwa  na wananchi wa Ruanda kwa sasabu ya vumbi za magari.....

Wednesday, September 20, 2017

TUKUMBUKE ZAMANI:- HISTORIA YA TAIFA LETU KATIKA PICHA.......

DAR ES SALAAM:- WANAWAKE WAFUNGWA WAKITENGENEZA BARABARA
ASKARI WAPO KATIKA GWARIDE  KATIKA HOSPITAL YA OCEAN ROAD 

Tuesday, September 19, 2017

VITU VYA ASILI NI BORA ZADI KULIKO VYOVYOTE VILE...TUVITHAMINI...NI KAZI ZA MIKONO YETU TUKUMBUKE

 MIKOBA YA ASILI
BANGILI
TUDUMISHE UTAMADUNI WETU/VITU VYETU VYA ASILI ILI KIZAZI KIJACHO KIJE KUJUA HAYA. NAWATAKIENI KILA LA KHERI...

Monday, September 18, 2017

WIKI HII NI WIKI YA KUMBUKUMBU: ANGALIA HIINIMEIKUTA KWA MDOGO WANGU KOERO MKUNDI AKISEMA, DADA YASINTA NIMEISHITUKIA JANJA YAKO....ENDELEA

Dada yangu akiweka mikakati
Kwa dada yangu Yasinta,

Nimesikitishwa sana na kile ulichobandika katika blog yako ukidai kuwa wewe hutaki kuwa mwanaharakati wa kututetea sisi wanawake na watoto zetu, kama nilikunukuu vizuri umesema kuwa kuandika kwako makala za kutetea haki za wanawake sio kwamba unayo dhamira ya kuanzisha NGO.

Umedai kuwa hujawahi kuota na wala kuwaza kufanya kazi hiyo, bali unaamini kwamba, kuwa mwanaharakati haimaanishi kuwa na Organization. Kwamba huwezi kuwatetea wanawake na watoto isipokuwa mpaka uwe na NGO.

Pia ukabainisha kuwa umeamua kuweka mambo hadharani maana kuna vimbelembele washaanza kujifanya yule shehe wa Mwembe chai aliyetabiri kuwa mwana CCM yeyote atakayechukua fomu za kutaka kugombea urais kwa kumpinga Rais wa sasa Muheshimiwa Kikwete basi atakufa ghafla kwa kubanwa na ngiri. Vimbelembele hao wamekutabiria kuwa kwa kuandika kwako vimakala vya kujifanya una huruma sana na wanawake wanaonyanyaswa na waume zao ni kamchakato kako ka kuelekea kuanzisha Organization ya kuwatetea wanawake nchini.

Duh! Samahani dada nilisahau kukupa heshima yako. Nakupa shikamoo zako wewe na mumeo. Habari za huko ughaibuni mlipo, nasikia kuwa kuna baridi sana kiasi kwamba mabarafu yamejaa kila mahali mpaka chooni. Samahani kwa kutaja chooni, nimesahau kuwa hilo sio neno la kistaarabu, nilikuwa namaanisha toilet.

Dada kama nilivyoanza katika utangulizi wa barua hii, ni kwamba nimeishitukia janja yako. Unajua tangu uhamie ughaibuni dada umekuwa na akili sana.

Sio wewe mwaka juzi ulipokuja huku nyumbani ulianzisha NGO ya kutetea haki za wanawake na watoto kwa kushirikiana na yule binamu yako anayezaliwa na yule shangazi, ambaye analazimisha undugu baada ya kusikia kuwa umeolewa na mzungu kwa kudai kuwa eti zamani alikuwa akimbeba baba yako wakati bibi na babu yako wakienda shamba.

Huyu binamu yako ambaye inasemekana alifeli zaidi ya mara saba kuingia kidato cha pili huko Songea katika ile shule iliyoko pale Mfaranyaki, karibu na ule muembe dodo unaotumiwa na mafundi baiskeli ndiye uliamua kumshirikisha kuanzisha NGO yenu wenyewe ambayo mliipa jina la Ruhuwiko NGO for woman and children crying everyday.
Taasisi hiyo ambayo imesajiliwa na katibu kata ilikuja kwa kasi ya ajabu na inatishia kuvunja ndoa za watu, na mojawapo ya ndoa iliyovunjika ni ile ya yule mzee Ngatura mwenye wake saba.

Ndao iliyovunjika ni ya yule binti machepele wa saba kuolewa na yule mzee. Nadhani unamkumbuka yule binti aliyewahi kufumaniwa na mke wa mwalimu wa kufundisha ngoma za asili pale shuleni, na kutokana na umahiri wa kucheza lizombe yule binti alipewa Umanju wa kuongoza ngoma na mwalimu na kutokana na kupewa cheo hicho mwalimu wa ngoma akamgeuza kuwa kijumba kidogo chake na makutano yao yakawa kule kwenye shamba la kijiiji, na kama unavyojua wambea wa kijiji wakamjuza mke wa mwalimu wa ngoma na hivyo kuwekewa mtego na kufumaniwa. Si unakumbuka jinsi alivyopigwa mpaka akachaniwa nguo zote? Basi kutokana na aibu si ndio akahamishiwa katika shule ya jirani na baba yake ili kukwepa aibu.

Basi huyu binti baada ya kuachika huku akiongozwa na binamu yako wanataka mali za yule mzee zigawanywe sawa kwa sawa la sivyo kesi inapelekwa mahakaam kuu.
Hivi ninavyo kuandikia kuna mashauri zaidi ya wanawake 30 wanaotaka kuachana na wanaume zao kwa kutegemea kugawana mali walizochuma na wanaume zao. Kampeni hiyo ya kuachanisha wanandoa inaongozwa na hiyo NGO yenu na anayeingoza uasi huo wa kuvunja ndoa za watu ni huyo binamu yako.

Hivi sasa hali ni tete pale kijijini na wazee wa kijiji wameitisha kikao cha dharura kujaldili hali hiyo na wanatishia kuchangishana nauli ili waje Dar kumuona muheshimiwa rais ili anusuru ndoa zao zinazoelekea shimoni. Pia wanataka binamu yako huyo aondolewe haraka pale kijijini kwa ile staili ya kuwekewa karantini asikanyage tena pale kijijini iwe ni kwa sherehe au misiba.

Hata hivyo katika utetezi wake binamu yako huyo amejitetea kuwa eti hiyo kampeni ya kuachanisha ndoa za watu ni idea yako yaani kwa kiingereza suggestion yako maana alidai kuwa yeye siye msemaji mkuu wa hiyo NGO, bali ni mtekelezaji wa kile unachokiagiza ukiwa huko ughaibuni.

Sasa dada kwa kutaka kutuchota akili unajidai kuwa hutaki kuwa mwanaharakati wakati tayari ulishakuwa mwanaharakati tangu mwaka juzi. Kwa kuwa unatafuta umaarufu ili kutengeneza mazingira ya kupanua wigo wa hiyo NGO yako kutoka kijijini hadi kuwa NGO ya kitaifa baada ya kuona kule Ruhuwiko umeanza kupoteza umaarufu na ndio maana unataka kupata maoni ya wasomaji wako katika ile staili ya mchomeko, yaani ku bip kwa kiingereza.

Dada samahani naomba univumilie kwa haya ninayoyasema maana mie sitaki uje kuumbuka baadae, kwani Dar es salaamu sio sawa na Ruhuwiko, huku kuna ushindani wa hii biashara ya NGO, usipoangalia utatapeliwa wewe, kuna watu huku ni wasanii ile mbaya, anaweza kuja mwanamke akajidai amegombana na mumewe, na akipata msaada huyooo anaenda kuendelea na ndoa yake kama kawaida. Ukitaka kupanua wigo wa NGO yenu ihamie huku Dar inabidi utafute mganga ambaye anaweza kumwangalia mteja akajua kama huyu ana matatizo kweli au msanii tu.
Dada huku Dar NGO ni mradi wa watu wajanja ambao hutumia staili ya matatizo yenu ndio tijara yetu, na wengi wao ni wale walioshindwa kutofautisha ile dhana kujiajiri na kujitolea. Kwa wao kuitolea maana yake ni kuwekeza kwa kutumia matatizo ya wengine.

Yaani siamini kuwa na wewe umeingia katika kamtindo hako kwa kutafuta fedha kwa kutumia matatizo ya wengine. Nashawishika kuamini kuwa na wewe umefulia kimawazo, kwani hiyo mbinu yako nimeishitukia dada. Hapa Dar humpati mtu labda Kamala na Chacha kwani nao eti ni wanaharakati wa kuwatetea vijana…….LOL

Kwa leo naomba niishie hapa nikipata muda nitakujuza mengi juu ya NGO za hapa Dar.

Nakutakia siku njem

Friday, September 15, 2017

ZILIPENDWA KWELI NI DHAHABU...VAZI LA MAUA-MAUA NA MKANDA JUU....

Nimekumbuka sana zamani...ebu angalia hii picha. Sijui ilikuwa ni mtindo kusimama kwenye miti au maua..? Maana nimejiuliza hata jibu sijapata.  Na pia mtindo wa nyweleJe? mnamfahamu huyu mdada?
IJUMAA NJEMA KWA ATAKAYEPITA HAPA!

Thursday, September 14, 2017

PICHA MOJA MWONEKANO TOFAUTI...SWALI JE? MWONEKANO UPI WAMFAA DADA HUYU?

Kwanza ilikuwa hivi ....Baadaye dada yangu Mariam akaona kuna vitu vinakosekana  kama uonavyo  alivyoorodhesha katika picha....
Miaka imepita na jana ndipo nilipotumiwa hii picha kwa mfano huu. Hakika sikuitambua kabisa. Na bado sijitambui  maana hiyo si tabia yangu...Je wewe msomaji unauonaje huu mfano wa hii picha ya Kapulya ya mwisho?
NAWATAKIENI JIONI NJEMA KWA WALE WATAKAOPITA HAPA KIBARAZANI....KAPULYA MDADISI WENU

Tuesday, September 12, 2017

VYAKULA AVIPENDAVYO KAPULYA WENU ...AU KUNA MWINGINE ANAPENDA KAMA MIMI??

NI WALI NA KUNDE...KWETU UNGONINI TWAITA (NGUNDI MANGI)
Baada ya chakula nilipenda sana haya matunda ...kwa mara nyingine tena kikwetu twaita MADONGA....
Nikikosa hivyo basi nakula uyoga....Je wewe kuna chakula hujala siku nyingi na sasa watamani kukila? Nawatakieni wote jioni njema!!!

Monday, September 11, 2017

NI SIKU NYINGINE PIA WIKI NYINGINE NA NI JUMATATU....

Nawatakieni siju hii ya Jumatatu na wiki hii iwe yenye furaha na amani...pia nawatakieni yote mtakayofanya yawe yenye mafanikio mazuri.  PANAPO MAJALIWA TUTAONANA TENA !

Wednesday, September 6, 2017

SOKONI SONGEA... KUMBUKUMBU

Bado tuangalie Songea kwetu kama muonavyo hapa ni nje ya soko kuu la Songea.... TUONANE TENA WAKATI UJAO.

Tuesday, September 5, 2017

HII NGOMA WENZENU NIMEIPENDA IMEKAA KI-ASILI


PANAPO MAJALIWA TUTAONANA TENA...KAPULYA

Monday, September 4, 2017

TUANZE WIKI HII NA NENO FURAHA: HIVI KWANINI KUN SIKU MTU HUKOSA FURAHA?


Ndiyo...Furaha inatokana na ridhiko la ndani la mtu bila kuhusisha vitu vya nje. Mtu akishajua namna sahihi ya kuipata furaha basi hataipoteza kamwe. Yoyote anaeipoteza furaha huyo anakuwa anaitafuta nje yake kwenye mazingira ya nje.....
Lazima atakuja kuikosa siku moja kwasababu mazingura ya nje sio rafiki sana na binadamu kwasababu hubadilika badilika....

Mfano kuna wakati wa jua, masika na kiangazi za kawaida...
Kama umepanga kwenda kulipwa mapato yako fulani na umewekeza furaha yako kwenye hela halafu mvua ikanyesha lazima tu furaha yako itapotea....
Kuridhika kwa ndani kuna maana ya kujikubali jinsi ulivyo bila kutegemea hali ya nje iko namna gani...
Utakapo jikubali namna ulivyo kamwe hutajutia wala kukosa furaha hata siku moja

Saturday, September 2, 2017

UJUMBE WA LEO:- KILA AITAZAMAYE KESHO YAMPASA KWANZA AIMALIZE LEO:- ACHA NIKUDOKEZE JUU YA MAISHA YA LEO...

1.Ishi kwa UPENDO usio na Unafiki.
2.Ishi na FURAHA isiyo na mipaka.
3.Ishi kwa AMANI na kila Mtu.  
4.Usiweke MAMBO yako wazi kwa kila mtu kwani binadam hatufanani.
5.Jiheshimu kwani HESHIMA yako inatokana na jinsi ulivyo.
6.Kuwa MVUMILIVU katika kila jambo ili kufikia mafanikio.
7.Weka MSAMAHA mbele kwa kila anaekukosea na unaemkosea.
8.MISUKOSUKO ni sehemu ya maisha na ndio hatua ya kuvuka ili kufanikiwa katika MAISHA hivyo usikate tamaa.
9.Omba na kumshkuru MWENYEZI MUNGU kwa kila jambo kwani yeye ndiye anayekupa UHAI.
TUMALIZIE NA WIMBO HUU ....